Barua ya wazi ya mzee Joseph Butiku kwenda kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan

Mheshimiwa Rais, ninayo heshima kubwa kukuandikia kuhusu masuala vanayohusu maslahi ya nchi yetu na Chama chetu kwa jumla. Rais ni taasisi, na inaweza kuonekana si sawa mimi kukuandikia moja kwa moja badala ya kuanza na wasaidizi wako. Kwa umri niliofikia, na kwa imani kubwa niliyonayo kwamba wewe ni msikivu, na kwa kuwa naandika kuhusu masuala yenye maslahi kwa hai na uimara wa Chama chetu, nimeonelea nikuandikie wewe moja kwa moja.

Nianze moja kwa moja kwa kusema yafuatayo: la kwanza, nakuunga mkono kwa juhudi kubwa ya kuongoza nchi yetu kwa utulivu mkubwa tangu ulipochukua uongozi. Jambo la pili, chati ya Chama chetu imeshuka na kutishia pia kushuka kwa chati yako, jambo ambalo linaniogopesha na kunisukuma kukuandikia.
Natambua kwamba wapo watu watakaokuwa wanakueleza kwamba mambo ni mazuri. Kila kiongozi hakosi watu wa namna hii, ambao kazi yao ni kumpa habari njema tu, hata pale ilipokuwa dhahiri kwamba mambo sio mazuri. Hata Mwalimu Nyerere alikuwa nao. Mimi nafahamu kwasababu nimekuwa Msaidizi wake kwa miaka takriban 20. Hata pale tulipokuwa na mgao wa sukari, au pale nchi ilipokumbwa na njaa, na hata pale nchi ilipopitia misukosuko, wapo miongoni mwa wanasiasa waliokuwa wanamwambia Mwalimu kwamba mambo ni mazuri.

Naomba nirudie kwa msisitizo, mambo sio mazuri sana. Kazi nzuri umefanya, umetuongoza katika kipindi kigumu sana cha mpito, kutoka awamu moja iliyoisha ghafla hadi awamu mpya kwa busara na hekima kubwa. Miradi uliyoachiwa umeiendeleza na umeanza mingine na umeweka mkazo kwenye maendeleo ya jamii vijijini. Inasikitisha kwamba kunataka kufanyika makosa yatakayofuta mafanikio haya uliyoyaleta. Donda la makosa haya ni kuondoka kwa imani ya wananchi juu ya Chama chetu, juu yako na juu ya Serikali yako.

Imani ndio msingi wa uhalali wa utawala wowote. Imani ikishuka, hata tukiteleza llani kwa asilimia 100, bado tutakataliwa. Mwalimu aliongoza kukiwa na changamoto kwenye uchumi na watu walitaabika kidogo, lakini bado walimuamini.

Moja ya sababu ya kuporomoka kwa imani ni magomvi, fitna na kuchafuana baina ya viongozi. Pia dhana kwamba viongozi wanajinufaisha binafsi bila kujali wananchi wa kawaida na kwamba viongozi hawasikilizi wala kujali maoni ya wananchi. Haya yanaelekea kuanza kujitokeza miongoni mwa wananchi.
Changamoto ya Chama chetu siku zote haikuwahi kuwa kushindwa kutekeleza ilani. Siku zote tumefanya vibaya kwenye uchaguzi kwasababu ya kukosa umoja, kwasababu ya kugombana wenyewe kwa wenyewe. Kwa bahati mbaya, kutokana na ukubwa wa CCM, chama kikipasuka nchi nayo na taasisi mbalimbali nchini nazo zitapasuka.

Mimi ni mtu mzima, na ninakuheshimu sana kama kiongozi wangu, na kwamsingi huo ninawajbika kukuambia ukweli. Chama chetu kinaanza dalili za mpasuko. Mpasuko huo unatokana na maslahi binafsi. Tunaona na kushuhudia askari wa kukodi wakiingia msituni na kuanza kuchafua viongozi badala ya kujibu hoja na maswali ya msingi yanayoulizwa na wananchi kuhusu masuala mbalimbali. Tunaona jitihada za kukutenganisha na viongozi wenzako, watendaji serikali na baadhi ya watumishi wa umma, uwaone wabaya na wasio kutakia mema. Ipo vita kubwa ya kukumiliki baina ya makundi kisiasa ya huko nyuma ambayo wewe hukuwa sehemu yake. Wapo wafanyabiashara wanaolitumia vibaya jina lako, nafasi yako na hata kijana wako, kujijengea himaya sio tu ya kibiashara bali hata ya kisiasa. Kila zabuni inayofanywa na Serikali sasa hivi, na wawekezaji wengi wanapoingia nchini wanaambiwa watoe rushwa au hisa na wengine wanalazimishwa kutoa pesa za uchaguzi wa Mama 2025.

Nisingependa ushinde 2025 huku nchi, chama na wewe binafsi ukiwa na vidonda vingi kama ilivyokuwa mwaka 2015. Dali zinaashiria hivyo. Makovu ya vidonda hivyo bado tunayauguza hadi leo, na wapo miongoni mwetu ambao bado hawajapona hadi leo. Nakusihi, ujitahidi kukiendesha Chama chetu kwa ukweli kwa ukweli na uwazi. Wanaochafua wenzao na kuleta mpasuko wadhibitiwe kwani wanataka kukutumia kujenga himaya za maslahi yao binafsi. Njama na ujanja ujanja ufikie mwisho. Watu wenye sifa mbaya na heshima ndogo kwenye jamii, wakiisemea Serikali yetu wanatupaka matope yao. Waambiwe wake kimya. Usiwape nafasi ya kukuteka wewe na serikali yako (state capture).

Maoni haya nimeyatoa kwa nia njema kwa maslahi ya kulinda heshima yako, nafasi na kiti chako kama Rais, chama chetu na nchi yetu.

Wako katika Ujenzi wa Taifa,

Joseph Waryoba Butiku